Sunday, September 9, 2012

Umewahi kumsikia mwanadamu huyu?


ANAWEZA kuwa katika ufukwe wowote kwa sasa, sigara ikiwa mdomoni, whisky kando yake, laptop pembeni na simu mkononi akiwasiliana na wateja wake.
Miongoni mwa wateja wake ni kocha wa soka maarufu zaidi duniani kwa sasa, Jose Mourinho au wanasoka mahiri Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Maisha yanataka nini zaidi unapokuwa na wateja hao?
Hapa namzungumzia mtu anayeitwa Jorge Mendes, raia wa Ureno. Umewahi kumsikia mtu huyu? Wengi hawamfahamu.
Binafsi namfuatilia.
Ananikosha sana. Ni wakala wa Ronaldo na Mourinho. Hilo si jambo kubwa sana, anachonikosha ni namna ambavyo anawamiliki wachezaji wengi wa Ureno na Brazil ambao wanatamba kwa sasa. Sijui aliwapataje!
Ndani ya mastaa hawa, yeye ndiye mtengenezaji wa dili zao zote.
Yeye ndiye anahusika kuwahamisha. Simu za akina Roman Abramovich, Sir Alex Ferguson, Fiorentino Perez, Masimo Moratti na wengineo zote huwa zinamngoja yeye.
Wateja wake wengine ni akina Luiz Felipe Scolari, Simao Sabrosa, Anderson, Fabio Coentrao, Pepe, Angel Di Maria, Radamel Falcao, Ricardo Carvalho, Louis Nani, Ricardo Quaresma na wengineo.
Yeye ndiye alikuwa mchezeshaji wa dili la Ronaldo kutoka Sporting Lisbon kwenda Manchester United. Hakukosa pauni 1 milioni ya kuweka mfukoni.
Bado akaendelea kuwa wakala wa Ronaldo alipohama kutoka United kwenda Real Madrid, Mendes alikuwa na chake �cha juu�.
Uhamisho ulikwenda kwa pauni 80 milioni, Mendes hakukosa pauni 5 milioni hapo.
Ndio maisha yake. Wakati Anderson alipohamia Man United kutoka Porto, Mendes peke yake alilamba kiasi cha pauni 4 milioni. Porto, Anderson na Man United walijijua wenyewe.
Kila anapokwenda Jose Mourinho ujue anakaa siti moja na wakala wake Mendes. Alipohama kutoka Porto kwenda Chelsea, yeye ndiye alicheza dili na Roman Abramovich.
Upande wa Mourinho yeye ndiye aliyechezesha mchezo, upande wa Chelsea, mwakilishi wao alikuwa mjanja mwingine anaitwa Pini Zahavi. Huyu Zahavi nilishawahi kumwandika hapa.
Mendes alimeza pauni milioni kadhaa za Abramovich na baada ya Mourinho kufukuzwa na Abramovich, Mendes ndiye aliyekuwa dalali wa Mourinho kwenda Inter Milan kwa tajiri mwingine, Massimo Moratti.
Baada ya Mourinho kuondoka Inter Milan, yeye ndiye aliyesimamia dili la Mourinho kwenda Real Madrid kwa tajiri mwingine, Fiorentino Perez.
Ebu jiulize, kama umewahi kufanya biashara ya kumuuzia mtu, Abramovich, Moratti na Perez utakuwa umeingiza kiasi gani? Maisha yanataka nini zaidi?
Majuzi wakati mashabiki wengi wakishangilia mabao ya Falcao dhidi ya Chelsea, nilikuwa nimejibanza baa moja inaitwa Etina pale maeneo ya Survey jijini Dar es Salaam nikifikiria jinsi ambavyo Mendes anacheka kwa sasa akiona jinsi biashara ya Falcao itakavyokuwa tamu.
Yeye ndiye alisimama katika dili la Falcao kutoka Porto kwenda Atletico Madrid, sasa matajiri wa Man City na Chelsea wote wanamhitaji Falcao kwa udi na uvumba. Hata hivyo hawawezi kumpata Falcao mpaka kwanza wapige simu ya mkononi ya Mendes.
Unadhani ataingiza kiasi gani? Falcao ana thamani ya pauni 50 milioni. Mendes ndiye ataendesha biashara na hakosi pauni 4 milioni. Dunia ya sasa hauwezi kumpata Falcao, Mourinho, Ronaldo wala Luis Nani bila ya yeye.
Raha iliyoje!
Majuzi Ronaldo amelalamika kuwa hana furaha na Real Madrid na anataka kutimka. Kitu cha kwanza alichofanya Rais wa Madrid, Perez ilikuwa ni kupiga simu kwa Mendes kuuliza kama mteja wake alikuwa amepata ofa yoyote. Mendes alijibu hapana.
Lakini ni wazi kwamba anasikilizia. Ametega masikio kwa tajiri wa Kiarabu wa Man City. Kama lolote likitokea, uhamisho wa Ronaldo utavunja tena rekodi ya uhamisho duniani.
Safari hii Mendes atavuna noti nyingi zaidi kwa mkupuo ambazo hajawahi kuzivuna katika maisha yake. Sidhani kama atakosa pauni 10 milioni kwa dili nzima.
Huyo ndiye Mendes. Kila siku, Nani anahusishwa kuhama United, Mendes ana pesa yake. Hata kama akisaini mkataba mpya, bado ana dau lake kutoka kwa Nani. Mendes ndiye ataongea na akina David Gill wa Man United.
Wakati mwingine huwa nahisi kuwa anacheza dili na Mourinho kwa baadhi ya wachezaji wa Kireno anaowamiliki.
Wakati Mourinho alipohamia Chelsea na kuleta kundi la wachezaji wa Kireno, Thiago, Ricardo Carvalho, Paulo Fererra na Maniche, wote hawa walikuwa chini ya uwakala wa Mendes.
Nilijaribu kufuatilia historia ya huyu Mendes. Jamaa amepitia maisha yale yale ya chini ambayo watu wengi wa mpira wanapitia.
Kwanza alikuwa DJ, baadaye akafungua duka la kukodisha filamu, baadaye akafungua baa kisha klabu ya usiku katika eneo la Caminha huko kwao Ureno.
Lakini sasa nadhani anakula kuku kwa mrija. Kama unawamiliki Ronaldo, Mourinho, Falcao, Nani, Di Maria na wengineo, maisha yanazidi kuwa rahisi hasa wakati huu ambao unajua muda wowote utakuwa dalali wa Falcao na zaidi katika wakati ambao Ronaldo anatishia kutimka Madrid.
Si ajabu mpaka muda huu ninapoandika tayari simu yake iko bize kuzungumza na wakala wa Masheikh wa Man City. Nani anabisha?

No comments:

Post a Comment