Tuesday, September 11, 2012

DC amkwida diwani katika chakula

AAAAA
MKUU wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, juzi alimkwida na kumuondoa katika mstari wa viongozi kwenda kupata chakula, Diwani wa Kata ya Nyihogo (Chadema), Amos Sipemba.
Chakula hicho kilikuwa maalum kwa msafara wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Katika tukio hilo lililotokea wakati wa chakula cha mchana katika viwanja vya nyumba ya mapumziko alipokuwa amefikia waziri mkuu, Mpesya alianza kuwakaribisha wageni wa kimkoa kutangulia kupata chakula, huku akiwataka baadhi ya viongozi wa wawakilishi wa wananchi ,kuungana na msafara huo.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye alionekana kuwa makini zaidi na ugeni huo, akiwa mara yake ya kwanza kupokea ugeni wa kitaifa tangu aipoteuliwa miezi minne iliyopita, alisimamia ugawaji wa chakula kwa wageni na wenyeji waliokuwa katika msafara huo.
Baada ya kumaliza kutangaza wageni wa kimkoa, aliwachagua Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Machibya Jidulamabambasi na makamu wake, Lucas Makulumo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya wa Kahama, Alfred Mahanganya na makamu wake Mibako Mabubu.
Hali kadhalika Diwani wa Kahama Mjini ili waungane na msafara huo katika upata chakula.
Diwani Sipemba akiwa na mwenzake wa Kata ya Mwendakulima (TLP), Ntabo Majabi nao walijipachika kwenye mstari wakiwa nyuma ya Diwani wa Kata ya Kahama Mjini, Abasi Omari, ambaye Mpesya alimtaka ajumuike na ugeni kutoka mkoani.
Lakini alipoona Sipemba yuko mstarini, mkuu huyo wa wilaya alikwenda na kumtaka asiingie kwenye mstari lakini diwani huyo alikaidi amri.
Kitendo hicho kilimfanya Mpesya ampige jeki kwa nyuma kwa kutumia mkanda wa suruali aliyokuwa amevaa (diwani) na kumnyanyua mithili ya mhalifu.
Hatua hiyo ilimwezesha kiongozi huyo kufanikiwa kumuondoa diwani huyo kwenye mstari wa wageni na kumrejesha nyuma ambako alidakwa na askari polisi waliokuwa wakilinda usalama katika eneo hilo.
Hata hivyo baadhiya madiwani walilalamikia kitendo hicho walichokielezea kuwa ni cha udhalilishwa kwa mwenzao hasa baada ya kubaini kuwa diwani mwenzie wa TLP aliyeingia naye kwenye mstari, aliachwa mstarini.
Baada ya malalamiko hayo, mkuu wa wilaya alikwenda tena kwenye mstari wa wageni wa kimkoa na kumtaka diwani aliyekuwa amebaki kwenye mstari, atoke na alifanya hivyo.
Alisikika akisema mara nyingi madiwani wamekuwa wakivuruga itifaki katika misafara ya wageni wa kitaifa na kwamba sasa lazima waheshimu na kufuata taratibu.
Hata hivyo wakati ugawaji chakula ukiendelea mkuu huyo, alimfuata diwani huyo na kumnasua kutoka kwenye mikono ya polisi waliokuwa wamemshikilia.
Alimpeleka ndani ya ukumbi na kumuinganisha na wageni katika kupata chakula, jambo ambalo watu walilitafsiri kuwa ni kujisafisha baada ya kumdhalilisha diwani.

No comments:

Post a Comment