Wednesday, September 5, 2012

Majibu 4 ya Waziri Nchimbi alipoulizwa maswali kadha kuhusu msiba wa Mwangosi

112Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alipoulizwa:
Kama yuko tayari kumsimamisha kazi Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda ili kupisha uchunguzi huo alisema ndani ya tume hiyo kuna Naibu Kamishna wa Polisi; hivyo kamanda huyo ambaye cheo chake ni Kamishna Msaidizi hana ubavu wa kuharibu uchunguzi huo.
Kuhusu askari aliyempiga bomu Mwangosi kama anashikiliwa na Polisi au bado yuko nje, alisema atachukua hatua mara baada ya tume hiyo au ile ya Polisi, iliyoundwa na Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema kukamilisha uchunguzi wake.
Kuhusu kama atajiuzulu iwapo ripoti itabaini kuwa polisi ndio waliofanya mauaji hayo, alisema “Nikijiuzulu mtampata wapi Waziri kama mimi? (kicheko) Shauri yenu… lakini nawahakikishieni kuwa ukweli utaanikwa wazi.”
Kwamba Polisi wanatumiwa kukikandamiza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kwa manufaa ya CCM, alisema hataruhusu hali ya namna hiyo na akasisitiza kuwa Polisi wamekuwa wanatekeleza agizo la Msajili wa Vyama vya Siasa la kupiga marufuku mikutano ya kisiasa katika kipindi hiki cha Sensa ya Watu na Makazi. Alipotolewa mifano ya namna ambavyo wanachama wa CCM wamekuwa wakifanya mikutano yake bila kuingiliwa na Polisi, Dkt. Nchimbi alisema alipata taarifa hizo na akamjulisha Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama ambaye alimhakikishia kuwa hakuna mkutano wa hadhara unaofanywa na chama chake badala yake wanafanya vikao vya ndani, “Mikutano ya ndani haikupigwa marufuku, kilichokatazwa ni mikutano ya hadhara na ninaomba wenzetu wawe wastahimilivu kwani zimebaki siku nne tu za sensa.”

No comments:

Post a Comment