Monday, September 10, 2012

Mwanafunzi auawa, achunwa ngozi

imagesMWANAFUNZI wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyarigamba iliyoko Kata ya Muhutwe wilayani Muleba, mkoani Kagera, Beatha James (12), ameuawa kikatili na kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vyake vya mwili na kung’olewa meno.
Mwili wa marehemu ambao ulipatikana baada ya siku nane maeneo ya kambi ya Jeshi la Wananchi Kaboya, ulikutwa umechunwa ngozi, shingo imekatwa, ulimi umetolewa, meno yameng’olewa, sehemu zake za siri zikiwa zimeondolewa na kunyolewa nywele huku akiwa na matundu kichwani.
Kwa mujibu wa maelezo ya mama mkubwa wa marehemu, Eyudosia  Salvatory, aliyekuwa akiishi naye katika Kitongoji cha Bitende, mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani Agosti 29 mwaka huu majira ya saa 3.30 asubuhi akielekea kwa mama yake mdogo mwingine aitwaye Mariagoleti Ishengoma.
Eyudosia alisema baada ya kufika huko alitumwa akafuate maziwa kwa jirani yao aitwaye Erasmo Sostenes, lakini akatumia muda mrefu bila kurejea ndipo walipopiga simu sehemu wanayochukua maziwa  wakaambiwa kuwa hajafika na maziwa bado hayajachukuliwa.
Alisema ilipofika saa saba za mchana walianza kumtafuta ndipo alijitokeza mama mmoja aliyemtaja kwa jina la mama Anneth, akawaeleza kuwa  wakati akiwa shambani majira ya saa nne asubuhi alimuona Beatha akiwa amefuatana na mwanaume mmoja aliyekuwa amebeba mfuko wa ‘safulet’ akamuuliza anakwenda wapi, akamjibu kuwa anamwelekeza mwanaume huyo njia ya kwenda Maziba ziwani maeneo ya Bubabo.
Aliongeza kuwa wananchi waliamua kufuatilia njia hiyo wakishirikiana na wanafamilia kumtafuta mtoto huyo na walipofika Maziba walielezwa kuwa walimuona akiwa amefuatana na mwanaume, lakini hawakujua walikoelekea.
Kwamba wakati  wakielezea  wasifu wa  mwanaume  anayedaiwa  kumchukua mtoto huyo, walielezwa kuwa watu  hao wanatunzwa  kwenye nyumba ya mkazi wa eneo hilo waliyemtaja kwa jina la Jacob na wakati wakielekea huko walikutana na mtoto wake ambaye alikimbilia kwa baba yake.
Eyudosia alifafanua kuwa walipofika kwa Jacob walimhoji ataje walipo watu anaoishi nao, lakini akadai hajui walipo kwani walifika hapo kutafuta kazi na kwamba mmoja wao alimueleza kuwa ana dili la fedha la kwenda kuiba mabati maeneo ya Igurubiri.
Wananchi hao walimchukua Jacob hadi eneo la Muhutwe akiambatana na mtoto wake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 13, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba, na kwamba walipombana alikiri kuwa mwanaume huyo anayetafutwa alifika kwao akiwa na binti, wakalala lakini waliondoka usiku akiwa ameshikwa na vijana.
Eyudosia alisema kuwa baada ya maelezo hayo, walipiga simu polisi ambao walifika na kumpeleka Jacob kituo cha Muleba kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa mtoto.
Alisema Septemba 7 mwaka huu, ndipo walipopata taarifa za kupatikana maiti ya mtoto huyo katika maeneo ya Kaboya karibu na kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwamba taarifa za mwili huo zilitolewa na wawindaji wanaowinda wanyama waharibifu na kuwa walipofika walikuta mwili wa Beatha ukiwa umechunwa ngozi, shingo imekatwa, ulimi umetolewa, meno yameng’olewa, sehemu zake za siri zikiwa zimeondolewa na kunyofolewa nywele huku akiwa na matundu kichwani.
Alisema sura ilikuwa imeharibika hivyo waliweza kumtambua kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa kabla ya kukutwa na mauti.
Mtendaji wa kijiji hicho, Dominic Damasenyi, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba taarifa zilitolewa kwake na wanafamilia.
Damasenyi alisema madaktari walifika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi mwili huo kisha wakaruhusu shughuli za mazishi kuendelea.

No comments:

Post a Comment