1. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko
makubwa kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha
Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.
2. Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa
Habari mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa akiwa kazini jana, Septemba 2,
2012, wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
3. Tukio hili linaiingiza Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na
ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza
tunashuhudia mwandishi wa habari AKIUAWA WAKATI AKITEKELEZA MAJUKUMU
YAKE YA KIHABARI.
4. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Mwangosi kabla ya kufikwa na
mauti saa 9.30 alasiri katika kijiji cha Nyololo, Mufindi, alizingirwa
na kushambuliwa na polisi waliokuwa katika eneo la tukio. Na hata
alipopiga kelele za kuomba msaada, hakusikilizwa na matokeo yake aliuawa
na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.
5. Kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, TEF tumechukua hatua
za haraka za kuunda timu ya uchunguzi wa suala hilo, ambayo itakwenda
mkoani Iringa mapema kadri itakavyowezekana, ili kubaini ukweli wa tukio
hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi
(documentation) ya tukio hilo la aina yake katika historia ya nchi yetu.
6. Matokeo ya uchunguzi huo pamoja na mwingine unaofanywa na Umoja wa
Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ndiyo yatakayotoa
mwelekeo wa hatua ambazo TEF inachukua dhidi ya Jeshi la Polisi katika
siku chache zijazo.
MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF
Kwa kuzingatia taarifa kutoka Iringa na zile za vyombo vya habari vya
jana (Jumapili, Septemba 02, 2012) na leo (Jumatatu, Septemba 03,
2012), TEF ina mtizamo na msimamo kama ifuatavyo:
1. Kwanza tunalaani vikali tukio la kupigwa, kisha kuuwawa kwa
mwandishi Daudi Mwangosi ambalo limeigusa tasnia ya habari kwamba sasa
pengine waandishi wa habari ni malengo “target ya polisi” wanapokuwa
kwenye kazi zao.
2. Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya
waandishi wa habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo
cha uhasama na ufa mkubwa ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa
na pande mbili ambazo zinategemeana.
3. Kwa matukio ya aina hii, tunadhani wakati mwafaka kwa uongozi wa
Jeshi la Polisi nchini kuwajibika, kuazia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa
na uongozi wa Makao Mkuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi
Mwema.
4. Tunasema hivi kwani kuna kila dalili kwamba polisi wanahusika kwa
namna moja au nyingine na tukio au/na matukio yaliyosababisha kifo cha
Mwangosi, kwani kitendo cha kumzingira tu na kumshambulia kinathibitisha
kwamba hawakuwa na nia njema hata kidogo dhidi ya mwandishi huyu.
5. Taarifa ambazo TEF tunazo, pia zinadai kwamba kulikuwa na mpango wa
polisi wa “kuwashughulikia waandishi wa habari watatu” (Mwangosi) akiwa
mmojawapo na hilo lilionekana likitekelezwa kwa polisi kumshambulia
mwandishi huyo, baadaye alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha
6. Hili linatiliwa nguvu na tukio jingine la polisi kumpiga na kumjeruhi
mwandishi mwingine, Godfrey Mushi ambaye ni mwakilishi wa gazeti la
Nipashe mkoani Iringa. Mwandishi wa tatu ambaye hadi tunapoandika
taarifa hiyo yumo katika mpango wa ‘kushughulikiwa na polisi’ ni Francis
Godwin ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.
7. Vitendo vya aina hii havivumiliki na havipaswi kuachwa kuendelea
kwani ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na uhuru wa habari nchini.
Hatuwezi kuendelea katika mazingira ambayo polisi wanageuka kuwa chombo
cha mauaji ya raia badala ya kuwa walinzi wa raia.
8. Kwa maana hiyo, mbali na uchunguzi ambao utafanywa na polisi, tunatoa
wito kwa Serikali kuunda chombo huru, ambacho kitabaini ukweli, na
matokeo yake yatangazwe kwa umma, huku wahusika wa aibu hiyo
wakichukuliwa hatua za kisheria. Tunasema hivyo, tukifahamu kwamba
tayari kuna jitihada za kuficha ukweli na kueneza propaganda za uongo
kuhusu tukio zima.
9. Mwenendo wa aina hii wa chombo cha dola kuamua kutumia silaha kuua
na baadaye kupanga mbinu chafu za kuficha ukweli ni hatari kwa Taifa,
na unaiweka demokraisia ya nchi yetu njia panda, huku tukielekea katika
hatari ya Taifa kutumbukia katika uovu.
No comments:
Post a Comment