Monday, September 10, 2012

Mrema: Nitaanza kuwachapa viboko wanywa gongo

images
MBUNGE wa jimbo la Vunjo, Dk Agustino Mrema amesema ataanza kuwachapa viboko wananchi watakaokamatwa wakiuza au kunywa pombe haramu ya gongo kwani inamaliza nguvu kazi ya taifa.
Mrema alisema amejitahidi kupiga vita uuzaji na unywaji wa pombe haramu ya gongo lakini kila wanapokamatwa na kufikishwa polisi wamekua wakiachiwa na kurudi mtaani kuendelea kuuza na kunywa pombe hiyo hivyo hana budi kuwachapa viboko mbele ya familia zao.
Akizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na mtandao wa mazingira mkoani hapa (Kenot) uliokuwa na lengo la kuibua changamoto za utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazosimamiwa na madiwani na mbunge, Mrema
alisema suala la ulevi kwenye jimbo lake umezidi kukua licha ya jitihada zinazofanywa na viongozi wa siasa na wa dini.
“Sasa mimi naona bora nianze kuwachapa viboko wajue yule Mrema wa 1991 ndio huyo huyo hajazeeka. Vijana wameharibika, asubuhi unakuta wamelewa gongo wengine mbundimbundi hawawezi kushika hata jembe maendeleo
yatatoka wapi kwa hali hii,” alisema.
Akizungumzia suala la uhamiaji haramu katika jimbo lake, Mrema alisema ziko njia za panya katika maeneo ya Taveta lakini akasema mtandao mkubwa uko kwa jeshi la polisi kwani kabla ya kufika Moshi vipo vizuizi vya polisi lakini wamekuwa wakipitishwa na polisi hawachukui hatua yoyote.
Alisema ni bora barabarani wakawekwa sungusungu watakaodhibiti magendo na wahamiaji haramu kuliko kuwaweka polisi ambao ndio wanawasafirisha kinyemela na kuliomba jeshi la polisi makao makuu kutazama upya utendaji wa kituo cha polisi himo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kenot anayeandaa midahalo hiyo kwa mkoa mzima, Pius Shirima alisema midahalo hiyo imefadhiliwa na Fondation for Civil Society na imelenga kuimarisha mahusiano na uwajibikaji kati ya madiwani, wabunge na wannachi kwa ujumla.
Alisema midahalo hiyo itasaidia kuweka mfumo ulio wazi na uwajibikaji ambapo wannachi watapata taarifa sahihi za mapato na matumizi na masuala mengine katika rasilimali zilizopo na pia itawafanya madiwani na wabunge kuhamasika na kuwa tayari kushirikiana na wananchi kutatua kero zao

No comments:

Post a Comment